Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepata ufadhili wa Shilingi Bilioni 66 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha  vituo vya Afya nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Hamisi Kigwangala Bungeni Mjini Dodoma allipokuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu, Khadija Nassir Ali juu ya utekelezaji wa agizo la Mwandoya la kuanzisha huduma za upasuaji katika vituo vyote vya Afya nchini.

Amesema kuwa, fedha za utekelezaji wa maboresho ya vituo hivyo zimeanza kupelekwa katika halmashauri husika ili kuanza maboresho katika vituo hivyo ambavyo vitarahisisha shughuli za upasuaji..

“Agizo la Mwandoya linazitaka  Halmashauri  nchini  kutumia fedha zao za ndani kuhakikisha zimejenga au kukarabati vyumba vya upasuaji kwa kipindi cha miezi Sita ili kupunguza vifo vya mama na mtoto na kupeleka huduma karibu na wananchi,” amesema Dkt. Kigwangala.

Ameongeza kuwa wataalamu wa Wizara hiyo kwa sasa wanatembelea vituo katika Halmashauri nchi nzima kwa ajili ya kufanya tathmini, kubaini waliotekeleza na ambao hawajatekeleza ili hatua za kinidhamu zifuate.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Wizara hiyo hadi sasa imesambaza vifungashio (delivery packs) 60,000 kwa mikoa sita (6) ya Kanda ya Ziwa ambayo vifo vingi vya mama wajawazito  na watoto vimekuwa vikitokea huko.

Bunge laziunganisha TRL na RAHCO
Mkuu wa Majeshi awatoa hofu wananchi