Serikali nchini, imesema inapendekeza kuondoa ada kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kupangiwa na Serikali kujiunga na vyuo vya ufundi vya Dar es Salaam Institute of Technology – DIT, Mbeya University of Science and Technology – MUST na Arusha Technical College
Pendekezo hilo, limetolewa Bungeni jijini Dodoma hii leo Juni 15, 2023 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha Bungeni mapendekezo ya ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/2024.
Amesema, “napendekeza kuondoa ada kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kupangiwa na Serikali kujiunga na vyuo vya ufundi vya Dar es Salaam Institute of Technology – DIT, Mbeya University of Science and Technology – MUST na Arusha Technical College – ATC.”
Dkt. Mwigulu ameongeza kuwa, hatua hiyo inalenga kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi na elimu inayohitajika katika zama hizi za mapinduzi ya nne ya viwanda (4th Industrial Revolution).
Amesema, Serikali pia inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kugharamia Programu hiyo ambapo hadi Aprili 2023 jumla ya shilingi bilioni 661.9 zimetolewa.
“Serikali imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 1.41 kwa wanafunzi wa elimu ya juu na pia imeendelea na maboresho ya miundombinu ya vyuo ikijumuishavyuo vikuu, vyuo vya ufundi stadi na vyuo vya maendeleo ya wananchi,” amesema Waziri huyo.