Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula amepiga marufuku utoaji vibali vya ujenzi wa viwanda katika maeneo ya makazi ya watu katika wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Dkt Mabula ametoa kauli hiyo jana, alipokutana na uongozi pamoja na watumishi wa sekta ya ardhi wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani Mkuranga mkoani Pwani kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi.
Amesema halmashauri ya wilaya ya Mkuranga lazima iandae Mpango Kabambe ambao utakuwa dira ya halmashauri hiyo kuonesha matumizi ya ardhi yake kwa kuwa maeneo kama viwanda, makazi na matumizi mengine yatakuwa yameoneshwa na kuondoa ujenzi wa makazi holela.
‘’Mkuranga lazima iwe na mpango wa matumizi ya ardhi unaoonesha viwanda vikae wapi, siyo viwanda kujengwa kila kona na katika mipango yenu halmashauri muandae maeneo yatakayowekwa viwanda’’ alisema Dkt Mabula.
Kuhusu zoezi la Urasimishaji, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameitaka Mkuranga kuharakisha zoezi hilo ili kuepuka makazi holela na kubainisha ucheleweshaji wowote utasababisha mji kutopangika na kusisitiza zoezi hilo lazima lisimamiwe kwa umakini.
Akigeukia suala la upimaji maeneo katika wilaya ya Mkuranga, Dkt Mabula alisema wilaya ya Mkuranga bado hajafanikiwa katika zoezi la upimaji pamoja na kuwa na viwanda vingi na kushauri wakati wa zoezi la upimaji lazima halmashauri iainishe pia maeneo ya uwekezaji.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mkuranga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega alisema, wilaya ya Mkuranga ina viwanda vingi kutokana kuwa na eneo linalovutia na kuongeza kuwa atafurahi kama Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi itafanya jitihada za kuharakisha zoezi la urasimishaji.
‘’Kama serikali itaongeza kasi kidogo ya kupanga na kurasimisha maeneo ya wilaya hii basi itakusanya kiasi kikubwa cha fedha maana Mkuranga imekuwa lango la ni kimbilio la wananchi kutoka Dar es Salaam kutokana na mkoa huo kujaa na mahali pekee pa kupumulia ni Mkuranga’’ alisema Ulega.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga, mhandisi Mshamu Munde alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa halmashauri yake ina migogoro mingi ya adhi ya kurithi na katika kukabiliana changamoto za ardhi ikiwemo makazi holela, tayari kuna Kampuni saba zinazofanya kazi ya urasimishaji na kusisitiza kuwa mkakati wa halmashauri yake ni kuzuia uanzishwaji makazi holela,
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga,Philberto Sanga amemtaka mtumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Mkuranga Welbert Mduma kujisalimisha mara moja wilayani humo, kujibu tuhuma zinazomkabili za kuhujumu mradi wa upimaji viwanja vya halmashauri ya wilaya ya Mkuranga katika maeneo ya Kikoo na Miale.
Mtumishi huyo ambaye ni Afisa Ardhi hajaonekana ofisi za halmashauri ya wilaya ya Mkuranga kwa muda mrefu tangu arejeshwe akitokea Morogoro alipohamishiwa baada ya kufanya ‘madudu’ katika mradi wa fidia ya ardhi katika maeneo yaliyopimwa viwanja na halmashauri ya Mkuranga.