Wizara ya maliasili na utalii imepiga marufuku wananchi kuuza nyama pori hadi ifikapo desemba mwaka 2019, ambapo kwa sasa wanaendelea kuandaa kanuni na taratibu, ambapo zikikamilika watatangaza kwa umma maeneo yatayowekwa mabucha.
Imeeleza kuwa itaendelea kudhibiti biashara hiyo, ili mwananchi aweze kununua nyama hiyo kwa njia halali.
“Haitachukua muda mrefu kanuni hizi zitatoka na tutatoa maelekezo watu wanaotaka kufungua hayo mabucha watayafungua kwa utaratibu gani” Amesema Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolfu Mkenda.
Akizungumza jana Jijini Arusha na vyombo vya habari Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolfu Mkenda amesema kuwa wizara itaendelea kudhibiti na kuhakikisha hakuna mwananchi hata mmoja atakayeruhusiwa kuuza nyama pori hadi pale serikali itakaporidhia.
“Sasa hivi tunapambana sana na ujangili wawanyama pori ambao wanakamatwa kwa mitego kaskazini mwa Serengeti, imeanza kuingia kidogo maeneo ya seluu, tunakamata watu sana lakini baadhi ya wenyeji wa kule nyama pori ni chakula chao cha asili” Amesema Profesa Mkenda.
Aidha amesema kuwa wanyama wote watakaowindwa kwaajili ya kuuzwa kwenye mabucha lazima wapimwe na waganga/Madaktari kwasababu wanyamapori wanamagonjwa mengi ambayo yanaweza kuleta athari kwa afya ya binadamu.
Hayo yamejiri baada ya Rais Dkt. John Magufuli akiwa mkoani Katavi kutoa maagizo kwa Wizara hiyo, huku akikumbushia maagizo ambayo alikwisha yatoa kwamba, ihakikishe inaanzisha mabucha ya kuuza nyama pori ili kuondoa na kudhibiti vitendo vya ujangili na kuwapa fursa wananchi waishio pembezoni mwa hifadhi kupata kitoweo kwa kuwa ni chakula chao cha asili.