Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema serikali itaanzisha kampeni ya kukagua Ofisi za Umma na binafsi ambazo zinatumia maziwa ya unga badala ya maziwa halisi yanayotengenezwa nchini.
Amebainisha hayo leo Mei 28 jijini Dodoma wakati akizindua wiki ya maziwa nchini ambayo itafanyika hadi Juni 1.
Ulega amesema ni jambo la aibu kuona watanzania wakitumia maziwa ya unga na kuacha yale yanayotengenezwa na watanzania wenzao jambo ambalo amesema siyo la kizalendo.
Amesema hakuna shida ya maziwa nchini kiasi cha wananchi kutumia maziwa ya unga na kueleza kwamba Tanzania inazalisha lita bilioni tatu kwa mwaka ambayo inatosheleza.
“Leo ukipita katika ofisi za Serikali karibu zote zinatumia maziwa ya kopo yanayozalishwa nje ya nchi, huu sio uzalendo, lazima tuwe wazalendo kwa kuanza kupenda vya kwetu, ifike hatua tuone aibu kwa ofisi tena za serikali kunywa maziwa ya kopo” Amesema Ulega.
Amesema sekta ya maziwa inachangia asilimia 1.2 ya pato la Taifa na kusisitiza unywaji wa maziwa kwa wingi utasaidia kutimiza ndoto ya Rais Dk John Magufuli kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
Amebainisha kuwa serikali imekua ikihangaika kutafuta vyanzo vipya vya mapato lakini kama fursa ya biashara ya maziwa itatumika vizuri basi Tanzania itapiga hatua kubwa sana kiuchumi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi amesema unywaji wa maziwa unachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha afya na kutoa rai kwa wananchi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla.