Serikali kupitia wizara zake nne, imelazimika na kuridhia kukabiliana na changamoto mbalimbali za utoaji wa huduma kwa wageni wanaoingia na kutoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) uliopo jijini Dar es Salaam.
Ambapo ametaja changamoto hizo ni pamoja na msongamano na joto katika eneo la kuchukulia mizigo, muda mrefu wa upatikanaji wa hati za kusafiria kwa wageni wanaoingia nchini pamoja na changamoto ya ufinyu wa eneo la kusubiri huduma uwanjani hapo.
Mawaziri wa wizara hizo walifikia azimio hilo jana baada ya kufanya ziara ya pamoja katika uwanja huo na kukagua shughuli za utoaji huduma.
Mawaziri hao ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dk. Susan Kolimba na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye.
Dk. Kigwangalla amesema amefikia hatua ya kukutana na mawaziri hao baada ya wageni, hasa watalii wanaoingia nchini, kulalamika kuwa wanatumia muda mwingi kuhudumiwa katika eneo la uwanja huo kiasi cha kuwapotezea muda.
Ameongeza kuwa kutokana na malalamiko hayo ya muda mrefu na mengine kadhaa, hatua mbalimbali zimechukuliwa tangu Agosti 8 mwaka jana wakati manaibu waziri wa wizara hizo nne walipofanya ziara uwanjani hapo.
Ambapo ameeleza kuwa wapo mbioni kutatua changamoto hizo kwa kuunda mikakati madhubuti kuboresha huduma katika viwanja vya ndege nchini ukiwemo JNIA.
Aidha amewaomba polisi wanaofanya kazi katika uwanja huo wa ndege kutotumia nguvu kukamata wageni kwani ni muhimu kumdhibiti mgeni bila kutumia nguvu..