Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amewaagiza Mameneja wa Wilaya, Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) nchi nzima, kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi Uviko-19 inakamilika kabla ya mwezi Juni mwaka huu.
Amesema kuwa hakutakuwa na nafasi ya maelezo kwa meneja yeyote ambaye atashindwa kukamilisha miradi hiyo kwa muda muafaka ambapo ameagiza miradi yote inatakiwa kukamilika Mei, mwaka huu.
Naibu Waziri huyo ametoa maagizo hayo leo Machi 2, katika siku yake ya kwanza ya ziara yake mkoani Simiyu, ambapo akiwa wilayani Busega amemtaka meneja wa RUWASA wilayani humo ambao wanatekeleza miradi miwili ya Uviko -19 kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
Amesema kuwa miradi yote ya Uviko-19 mbali na kukamilika ujenzi wake, inatakiwa kutoa maji na wananchi wanaanza kutumia na siyo kukamilika kwa kujengwa tu bali inatakiwa kabla ya muda huo ianze kutoa maji.
Amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameleta fedha hizo kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa Uviko, ambapo moja ya njia za mapambano ni wananchi kunawa mikono kwa maji safi na tiririka.
“Kunawa maji safi ambayo ni tiririka ni lazima kila miradi ukamilike ujenzi wake kwa asilimia 100 na siyo kukamilika alafu tunaambiwa kuna kitu fulani hakijakamilika, hapana…tunataka maji yatoke na wananchi waanze kutumia,” amesema Mhandisi Mahundi.
“Kwenye hii miradi kama wizara hatuna Excuse (msamaha) kwa Meneje yeyote wa Wilaya, wala hatuna muda wa ziada kwa ambaye mradi utashindwa kukamilika kwa muda, tunataka miradi ikamilike kabla ya mwezi wa tano na itoe maji kwa wananchi,” ameongeza Naibu Waziri hiyo.
Aidha, amewataka mameneja kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi wanaojenga miradi hiyo kwani muda uliobaki ni mchache sana na inatakiwa kukamilika ndani ya muda muafaka.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji ndani ya Wilaya Busega Meneja wa RUWASA wilayani humo Mhandisi Samson Gagala amesema kuwa walipokea zaidi ya Sh. milioni 450 fedha za Uviko -19 kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ya maji.