Serikali nchini, imejipanga kuhakikisha ugonjwa wa Ebola hauingii nchini, na kwamba tayari jopo la watalaam kutoka Wizarani wameweka kambi mkoa wa Kagera na maeneo mengine ya mpakani.
Hayo, yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma, kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Amalberga Kasangala hii leo Oktoba Mosi, 2022 Wilayani Bukoba mkoani Kagera, katika kikao cha dharura cha kujadili hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha ugonjwa wa ebola hauingii nchini.
Amesema, “Kutokana na tatizo ambalo limetokea nchi jirani tumeamua kuhamia hapa Kagera na timu ya watalaam kwani mkoa huu na mikoa mingine ya jirani zipo hatari zaidi na tumekaa kuweka mikakati mbalimbali ili kuuweka mkoa wa Kagera salama.”
Dkt. Kasangala ameongeza kuwa, njia sahihi ya kujikinga na ugonjwa wa ebola ni kuzingatia suala la usafi hasa kunawa mikono mara kwa mara na kwamba ni muhimu kuweka mikakati ya pamoja kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa wa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa wa ebola.
Naye, Mganga Mkuu Mkoa wa Kagera Dkt. Issessanda Kaniki amesema moja ya mikakati ambayo wameiweka katika mkoa wa Kagera katika kuzuia ugonjwa wa eboa usiingie nchini ni utoaji wa elimu nyumba kwa nyumba na kwa kusambaza vipeperushi na kuweka vifaa vya kupimia ugonjwa huo.
Akiwasilisha mikakati iliyoanza kuchukuliwa, mtalaam wa Elimu ya Afya kwa umma mkoa wa Kagera, Zablon Segeru amesema ni muhimu kuweka jitihada za kuizuia ebola huku Meneja Tume ya kikristo ya huduma za jamii CSSC, kanda ya ziwa Dkt. Andrew Cesari akisema upo umuhimu wa kuwashirikisha viongozi wa dini katika kuielimishaji kwa jamii juu ya kujikinga na ebola.
Katika kikao hicho, wajumbe wamependekeza namna ya kuzuia mipaka isiyo rasmi ambapo ipo zaidi ya 1200 mkoani Kagera, pamoja na mapendekezo ya kuweka matenti kila hospitali na kuweka mkakati wa kuzuia wafugaji wa kuhamahama kutoka nje ya nchi hususan Wanyankole kutoka Uganda.
Mlipuko wa Virusi vya Ebola, kwa mara ya kwanza ulitokea nchini Zaire (DRC), mwaka 1976 kwa kuwa na kesi 318, ambapo watu 280 walifariki na hivi karibuni umeripotiwa nchini Uganda ambapo hadi sasa kuna kesi 36 na ripoti ya vifo vya watu 23.