Serikali imekanusha taarifa za kuibwa kwa kompyuta za Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ikiwahakikishia wananchi kuwa compyuta za ofisi hiyo ziko salama pamoja na taarifa zake zote.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 19, 2019 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga amesema kuwa kompyuta zilizoibwa ni za ofisi ya mashtaka mkoa wa Dar es Salaam na sio ya DPP.

“Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka haikuguswa, nyaraka zote zipo, taarifa zote zipo na kazi yake inaendelea,”alisema Balozi Mahiga.

“Ofisi ambayo ilivunjwa ni ya mashtaka ya mkoa wa Dar es Salaam na baadhi ya kompyuta ambazo ni vipande tu. Hivyo vipande vya kompyuta ni sehemu ya vizibiti ambavyo polisi wanachunguza. Nataka kuwahakikishieni kwamba Ofisi ya DPP haijaathiriwa hata kidogo,” Balozi Mahiga amesisitiza.

Awali iliripotiwa kuwa ofisi hiyo imevunjwa na kwamba kompyuta zenye taarifa za kesi kubwa za uhujumu uchumi zimeibiwa.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa jana alikiri kupokea taarifa za wizi wa kompyuta zenye nyaraka za mashtaka na kueleza kuwa jeshi hilo limeanza kufanya uchunguzi.

Rais Magufuli afanye teuzi nyingine ya viongozi wanne
Utafiti: Kwanini wanaume wamekuwa wagumu kuoa, tunahitaji 'Upepo wa Kisulisuli'?