Saa chache baada ya Mahakama Kuu ya Gauteng ya Afrika Kusini kuamuru ndege ya ATCL iliyokuwa inashikiliwa katika uwanja wa Oliver Tambo iachiwe huru, Serikali imemshangaa mlalamikaji, Hermanus Stayn baada ya kubaini kuwa alifungua kesi nyingine hata kabla hukumu haijasomwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo nchini Afrika Kusini, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dkt. Damas Ndumbaro ameelezea jinsi ambavyo Mahakama Kuu imeamua na hatua zinazoweza kuchukuliwa baada ya hapo, lakini akaonesha kushangazwa na hatua ya mapema ya Stayn.

“Tumeshinda kesi hiyo, na imeamriwa kuwa ndege iweze kuondoka. Na kama kuna madai yoyote yale anapaswa kufungua kesi Tanzania. Walikuwa wakisema kwamba kuna maamuzi ya msuluhishi, lakini maamuzi hayo ya msuluhishi yameshabadilishwa na amri ya Mahakama,” alisema Dkt. Ndumbaro.

“Pamoja na hayo, bado Bwana Stayn ameshafungua kesi nyingine kupinga hukumu hii kabla haijasomwa. Na sisi tunashangaa sasa alijuaje hukumu hii itatoka dhidi yake yeye mpaka amekata rufaa tena hata kabla hukumu haijasomwa,” ameongeza.

Aidha, Dkt Ndumbaro ameeleza kuwa watalam wa Sheria waliokwenda nchini Afrika Kusini walikuwa wanajua wanachokifanya na kwamba licha ya maneno ya kejeli ya baadhi ya watu mitandaoni, alijua watashinda kesi hiyo.

“Sisi tulivyokuwa tunatukanwa mitandaoni tulikuwa tunaangalia tu, tulikuwa tunajua kazi tunayoifanya. Lazima ujue huku zimekuja PhD tatu,” alisema Dkt. Ndumbaro.

Katika kesi ya msingi, Steyn aliiomba Mahakama Kuu ya Gauteng kuizuia ndege hiyo ya ATCL aina ya Airbus A220-300 hadi pale atakapolipwa fidia ya dola milioni 33 kutokana na shamba lake lililotaifishwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 5, 2019
Sanchez aeleza kilichomsibu Manchester United