Kamati ya Bunge ya Ustawi wa Maendeleo ya Jamii, imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ustawi wa Vijana na Watu wenye Ulemavu kujikwamua kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatuma Toufiq kwenye kikao cha kamati cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana pamoja na utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Amesema, kamati hiyo itaendelea kuishauri Serikali kuendelea kuwezesha vijana kupata mikopo na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali, huku Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Prof. Jamal Katundu akisema ofisi hiyo imetenga Sh. 1 Bilioni za mfuko wa Watu wenye Ulemavu kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali za kundi hilo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako ameeleza kuwa Ofisi yake imefanya maboresho ya mwongozo wa mfuko huo mwaka 2023 ili kupanua wigo wa viwango vya mkopo inayotolewa sambamba na kumwezesha mtu moja moja kukopa badala ya kikundi.