Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwita Waitara amesema Serikali inatambua mchango wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (ALAT).

Waitara ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi kilichowakutanisha wajumbe wa Jumuiya za serikali za mitaa Afrika Mashariki (EALGA) kutathmini namna ya kuimarisha Mamlaka hizo.

Amesema Serikali inatambua juhudi zinazofanywa na mamlaka hiyo na imekuwa ikishirikiana na ALAT katika kuboresha masuala ya utawala bora, utoaji wa huduma, kuondoa umasikini ili kuhakikisha mpango wa maendeleo endelevu unafikiwa

“Tutaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na mamlaka hizo kwakua tunafanya kazi kwa karibu na mamlaka ya serikali za mitaa kuhakikisha sera ya ugatuaji wa madaraka itatekelezwa kwa asilimia mia moja,” amefafanua Waitara.

Amebainisha kuwa wao kama serikali wapo tayari kuchukua nafasi ya uenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za mitaa ya nchi za chi za Afrika Mashariki pindi nchi ya Rwanda itakapomaliza muda wake Mei 2020.

Aidha Waitara amewataka wanachama wa EALGA kutumia mkutano huo kubadilishana uzoefu katika maeneo ya utetezi, ushawishi, utoaji wa huduma na usambazaji wa habari zinazohusu Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa ya nchi za Afrika Mashariki (EALGA), Gulam Mukadamu amewaomba wakuu wa nchi wanachama ya Jumuia hiyo kuendelea kuhakikisha ugatuaji wa madaraka na kusaidia huduma za mitaa unakuwepo.

“Ni vyema EALGA ikaendelea kuwahimiza wakuu wa nchi wanachama wa utengamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuongeza juhudi za ugatuaji madaraka na kuongeza msaada wa kuboresha huduma za serikali za mitaa ili kuwa na taasisi iliyo imara,” amebainisha Mukadamu.

Hata hivyo Mukadamu ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kutekeleza Sera ya ugatuaji madaraka katika ngazi ya serikali za mitaa na kuwahimiza wahusika yakiwemo mabaraza ya madiwani kwa nchi wananchama kusaidia kuwekeza katika uimara wa EALGF na EALGA.

Vikwazo vyaibuka mpango wa nyuklia Rwanda
Waziri atishia kuifuta tume ya maendeleo ya ushirika