Naibu waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesisitiza nia na sera ya Serikali ni kuhakikisha Watoto wote hata wanaozaliwa kabla ya muda (njiti), walio chini ya umri wa miaka mitano wanapatia matibabu bure.
Dkt. Mollel ameyasema hayo Bunge jijini Dodoma, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Agnes Hokororo, huku akiwataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kusimamia utekelezaji wa sera hiyo kwenye maeneo yao.
Awali, akijibu swali la msingi la Mbunge wa Temeke (CCM), Dorothy Kilave aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kupeleka vitu muhimu vya kujifungulia akina mama, ili wasivinunue wakati wa kujifungua kwenye Hospitali na Vituo vya Afya.
Akijibu swahi hilo, Dkt. Mollel amesema Serikali imeweka sera ya kutoa huduma hizo bure lakini kuna baadhi ya maeneo vinakua havitoshi kutokana na wingi wa akina mama wanaojifungua huku akisema Bohari ya Dawa (MSD), tayari wameanza mchakato wa kupeleka vifaa hivyo.