Serikali ya Uingereza imetangaza kusitisha uajiri wa wafanyakazi wa afya kutoka nchini Nigeria, na kuliweka Taifa hilo kwenye orodha nyekundu ya mataifa ambayo watu wake hawataajiriwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya Shirika la Afya Duniani – WHO, kubainisha kuwa Nigeria ni miongoni mwa nchi 55 zenye changamoto kubwa ya wafanyakazi wa afya, katika ripoti iliyotolewa mwezi mmoja uliopita.
Aidha, Serikali ya Uingereza imewashauri waajiri wa afya na huduma za kijamii kutotafuta wafanyikazi kutoka nchi hizi isipokuwa pale ambapo kuna makubaliano kati ya serikali na serikali.
Mwaka 2021, Uingereza ilisitisha kuajiri wafanyikazi wa afya kutoka Nigeria na nchi zingine 46 ambapo kwasasa kuna madaktari 11,055 waliofunzwa kutoka Nigeria nchini Uingereza, kulingana na data ya Baraza Kuu la Matibabu la Uingereza.
Taifa la Nigeria, linashika nafasi ya tatu kwa idadi ya madaktari wa kigeni wanaofanya kazi nchini Uingereza ikiongozwa na India na Pakistan.