Serikali imefuta leseni zote za kuhodhi maeneo ya madini na wamiliki wake wametakiwa kuomba upya wakizingatia Sheria ya Madini na kanuni zake.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini nchini, Profesa Idris Kikula alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma, ambapo amesema kuwa tangazo la Serikali namba moja la mwaka 2018 limesema maeneo yote yaliyopewa leseni yanarejeshwa serikalini bila hakikisho la kupewa tena.

Amesema kuwa uamuzi huo umefanyika kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ikisomwa na marekebisho yake ya mwaka 2017 na kanuni ya 21 ya kanuni za Madini (Haki Madini za mwaka huu).

Aidha, amesema kuwa leseni zilizofutwa na wamiliki wake wanatakiwa kuomba tena zinazihusu kampuni 11, kwamba leseni hizo zinajumuisha migodi ya kati na mikubwa.

Migodi hiyo ni pamoja na Kabanga Nickel Company Limited, National Mineral Development Corporation Limited, Bafex Tanzania Limited ambayo inamiliki leseni za maeneo matatu.

Hata hivyo, mingine ni pamoja na Mabangu Mining Limited, Resolute (Tanzania) Limited, Wigu Hill Mining Company Limited, Nachingwea Nickel Limited na Precious Metals Refinery Company Limited.

 

Mwijage adai Propaganda zimekutana na 'Propagandist' aliyesomea China
Bashe: Mwijage amedumaza mazingira ya uwekezaji