Serikali imetaifisha tani 240 za mahindi na kuzigawa kwenye vituo vya watoto yatima na shule 18 za sekondari mkoani Songwe baada ya kuingizwa nchini kutoka nchi jirani kinyume na taratibu.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amekabidhiwa mahindi hayo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kufikia uamuzi wa kuyagawa baaada ya kujiridhisha kuwa yaliingia nchini kinyume na taratibu na sheria.

“Mahindi haya kisheria nimekabidhiwa baada ya wamiliki wake kushindwa kufuata sheria na taratibu za nchi yetu, yalitoka nchi jirani na yalikuwa yanapelekwa nchi nyingine jirani, TRA wameyataifisha na nimeona tuwagawie wanafunzi wetu na vituo vya watoto yatima wapate chakula kwakuwa mahindi haya tumejiridhisha pia kuwa yanafaa kwa chakula”, amesema Brig. Jen. Mwangelwa

Aidha, Meneja wa Ushuru wa Forodha wa Kituo cha mpakani cha Tunduma, John Masa amesema kuwa bidhaa zote zitakazobainika kusafirishwa kinyume cha taratibu zitataifishwa kama walivyofanya kwenye mahindi hayo baada ya kubaini kuwa yamesafirishwa kwa kukiuka sheria.

Kwa upande wao, baadhi ya wakuu wa shule za sekondari na wawakilishi wa vituo vya watoto yatima ambao wamepokea mahindi hayo ya chakula wameipongeza serikali kwa msaada wa mahindi ambao utasaidia upatikanaji wa chakula katika shule na vituo vyao.

 

Sugu aiponda sera ya elimu, awataka wadau kujitokeza
Video: Tundu Lissu amvaa tena Magufuli, Maagizo mazito, Mbwa wanasa shehena dawa za kulevya