Serikali kupitia Wizara ya Afya, imeainisha Mikoa mitano nchini iliyo katika hatari ya kupata mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ambao hivi karibuni umeripotiwa kuenea katika nchi jirani ya Uganda.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameyasema hayo hii leo Septemba 28, 2022 na kusema Mkoa ulio katika hatari zaidi ya kupata mlipuko huo ni Kagera ambao upo mpakani mwa nchi hiyo ambayo tayari imeripoti vifo vya watu 24.
Amesema, “Tumebainisha Mikoa mitano ambayo ipo katika hatari zaidi ya kupata mlipuko wa Ebola mkoa wa kwanza ni Kagera, na hii leo Katibu Mkuu wangu yupo Kagera kuangalia utayari wa Mkoa wa Kagera kukabiliana na mlipuko wa Ebola.”
Waziri Ummy ameongeza kuwa, “Wengi tunafahamu mabasi yanatoka Mtukula Uganda yanaishia Mwanza kwa hiyo Mwanza inaingia namba mbili katika kuwa kwenye hatari zaidi lakini pia kuna Kigoma, Geita na Mara.”
Aidha, amesema kwasasa wamebainisha Mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Kilimanjaro, Songwe, Mbeya na Dodoma kuwa katika hatari ya kati, kutokana na uwepo muingiliano wa watu katika Viwanja vya Ndege na vituo vikubwa vya mabasi kutoka nchi jirani.