Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo), Tixon Nzunda amewataka watendaji wa Serikali kufanya mabadiliko ya kifikra, kiutendaji na mifumo ya kiuendeshaji, ili kukuza sekta za uzalishaji mali nchini.
Nzunda ameyasema hayo Visiwani Zanzibar, wakati akifungua kikao kilichowakutanisha baadhi ya wataalamu wa Sekta ya Mifugo wa Wizara, taasisi na vitengo vinavyoshughulika na sekta hiyo kutoka Tanzania bara na Visiwani na kusema kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili hubeba uchumi wa nchi.
Amesema, “Watendaji serikalini wana wajibu wa namna ya kusimamia maslahi mapana ya nchi na lazima tuangalie ubora wa mifugo tunayoiandaa, tunayoifuga, mbari za mifugo zenye ubora unaotakiwa, madume yaliyo bora, lakini pia tija kwa maana ya kuongeza uzalishaji likiwemo la uhimilishaji.”
Aidha, ameongeza kuwa katika kuhakikisha sekta za uzalishaji mali zinakuwa na tija ni muhimu kuimarisha huduma za mifugo kwa maana ya afya ya mifugo, kinga ya mifugo, udhibiti wa magonjwa na kuimarisha miundombinu muhimu ya huduma ya mifugo.
Aidha, ameongeza kuwa, kikao hicho cha ushirikiano juu ya Sekta ya Mifugo ni muhimu katika kutatua changamoto zilizopo Visiwani Zanzibar na Tanzania Bara, ili kuwa na mwelekeo wa kuimarisha huduma za utafiti na ugani kwa upana.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Seif Shaban Mwinyi amesema moja ya nyenzo ya kupata rasilimali watu iliyo bora ni lishe na hususan unywaji wa maziwa yatokanayo na mifugo.