Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo katika machakato wa kukusanya maoni kwa wadau kutoka kanda saba za Tanzania bara yatakayowezesha kufanya maboresho ya sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia ya waka 2000.
Hayo yamebainishwa hii leo Novemba 6, 2019 Mkoani Singida na Mkurugenzi msaidizi idara ya sera na mipango kutoka Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Sophina Mjangu wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kilichowakutanisha wadau wa maendeleo ya wanawake na Jinsia toka mikoa ya Singida, Dodoma na Tabora na Wizara.
Amesema madhumuni ya sera iliyopo yalilenga kutoa mwelekeo ambao ungehakikisha mipango, mikakati na shughuli mbalimbali za uongozi ikiwemo maendeleo katika kila sekta na Taasisi yanazingatia usawa wa kijinsia.
“Lengo kuu la kupitia Sera hii ni kuifanya iendane na wakati na iweze kubeba mabadiliko yaliyojitokeza katika miaka kumi na tisa tangu kandaliwa kwake mwaka 2000 ikiwemo changamoto katika utekelezaji ikiwemo mapungufu na nini kifanyike ili kuiboresha kwa kueandana na wakati,” amebainisha Bi. Mjagu.
Akifungua kikao kazi hicho kwa niaba ya katibu tawala mkoa wa Singida, katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji, Stanslaus Choaji amesema kikao hicho kinatarajia kufikia malengo ya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake katika kufikia maendeleo jumuishi.
Amesema malengo hayo ni pamoja na Sekta ya afya, elimu, kilimo, fedha, uwezeshaji wa wanawake katika nafasi za uongozi, mazingira ya uzazi, afya ya mtoto na kukusanya taarifa ikiwemo takwimu zitakazowezesha kuandaa rasimu ya sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia.
“Pia kikao kazi hiki kitakusanya maoni yatayosaidia kuwa na sera shirikishi inayozingatia masuala yote muhimu na kupata uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wa Serikali na wadau katika uwepo wa sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia,” amefafanua Choaji.
Akiongea katika ufunguzi huo afisa maendeleo ya jamii mkoa wa Singida Jonathan Simiti amesema sera hiyo inatakiwa kufanyiwa maboresho na kwamba Serikali inafanya juhudi katika kuondokana na unyanyasaji wa kijinsia na ubaguzi ili iwasaidie wanawake kupata fursa mbalimbali za kiuchumi.
“Nimesikia kwenye vyombo vya habari kuwa wanawake sasa wanaendesha magari makubwa kama malori na mabasi ya abiria hii inaonesha kuwa masuala ya kijinsia yamekuwa kwa kiasi kikubwa nchini kwasasa” ameongeza Simiti.
Kwa upande wake Afisa Umustawi wa jamii mkoa wa Singida Shukrani Mbago amesema sera iliyopo ni nzuri na inatekelezeka ingawa kuna mambo muhimu yanatakiwa kuingizwa ikiwemo umiliki wa mali na kutoa maamuzi kwa watoto wa kike na wanawake katika ngazi ya Kata.
Serikali ipo katika kufafanya tathimini ya sera ya maendeleo ya wanawake ya jinsia ya mwaka 2000 na mkakati wa utekelezaji wake ili isaidie kufanya mapitio ya sera itakayozingatia makubaliano ya mikataba mbalimbali ya dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.