Serikali imewataka watalaamu wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi kuainisha mipango, mikakati na mahitaji ya vipaumbele vya shughuli za uhimilivu wa athari za mabadiliko ya tabianchi ili kuwezesha upatikanaji wa fedha za kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Switbert Mkama wakati akifungua Kikao cha Wadau kilichopitia na kuridhia andiko la kitaifa la programu ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kilichofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar Jijini Dodoma.
Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika ambapo hali hiyo inajidhihirisha kupitia matukio ya mvua zisizotabirika, ongezeko la joto, ukame na mafuriko na kuathiri sekta ya kijamii na kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo, maji, afya, nishati, misitu n.k
“Programu hiyo inatarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika wa Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kufanyika tarehe 4-6 Septemba, 2023 Nairobi, Kenya ili kuwezesha kutafuta fedha za kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dkt. Mkama.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Switbert Mkama (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa sekta ya umma na binafsi mara baada ya baada ya kufungua kikao cha wadau kilichojadili na kupitia kupitia Andiko la Kitaifa la Programu ya Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi kilichofanyika katika ukumbi wa St. Gaspar Jijini Dodoma Agosti, 2023.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Kemilembe Mutasa amewashukuru wadau na wafadhili waliofanikisha maandalizi ya andiko hilo na kuongeza kuwa Tanzania itahakikisha inatumia fursa hiyo kuhakikisha inachukua hatua madhubuti katika kuhimili athari za uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Kituo cha Kimataifa cha Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi – GCA Kanda ya Afrika, Dkt. Charles Nkemachena amesema Shirika hilo litaendelea kuziwezesha nchi za Afrika kupata ufadhili wa fedha za miradi ya kuhimili athari za mabadiliko kutokana na athari hiyo kuathiri mataifa ya Bara hilo.