Ili kuutendea haki Mpango Mkakati wa kutokomeza kero za migogoro ya ardhi ambayo imekuwa mwiba mchungu kwa wananchi na kuchafua taswira ya jiji kwa muda mrefu, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameitaka Halmashauri ya jiji la Dodoma na Kamati ya ardhi kufanya kazi kwa weledi.

Wito huo umetolewa wakati akizundua Mpango Mkakati wa Mkoa wa kushughulikia migogoro ya ardhi katika jiji la Dodoma, uliowahusisha Watumishi wa Halmashauri ya Jiji hilo, Madiwani, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Mkoa na Kamati ya Amani yenye wajumbe kutoka (dini mbambali) na vyombo vya habari. 

Amesema, “kwa muda mrefu Mamlaka mbalimbali za Serikali zimekuwa zikijitahidi kutatua migogoro hii lakini imekuwa haiishi na wananchi kuendelea kulalamikia Serikali. Kwa uchunguzi tuliofanya kama Mkoa tulibaini malalamiko mengi ni ya fidia na watu walioahidiwa kupewa viwanja mbadala. Kimsingi maelekezo mbalimbali yalikuwa yanatolewa ili kutafuta ufumbuzi wa suala hili.”

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa Uongozi wa Jiji wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatatua changamoto za ardhi zilizopo, kupitia Mkakati uliopangwa kutekelezwa kwa muda wa mwaka mmoja, ambao utekelezaji wake unaanza Julai 2023 na unatarajiwa kukamilika juni 2024.

Dkt. Tulia aongoza kikao athari mabadiliko Tabianchi
Tamaa ya mafanikio chanzo matumizi Dawa za kulevya