Serikali imetangaza kuanza kwa tahasusi (Combination) mpya tano kwa ajili ya Wanafunzi watakaoingia kidato cha tano mwaka 2021.
Lengo la kuongeza tahasusi hizo ni kuondoa changamoto ya ukosefu wa wataalam nchini ambayo imekuwepo kwa muda mrefu.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Seleman Jafo leo Jumatatu Machi 29, 2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Tahasusi hizo ni Fizikia, Hesabu na kompyuta (PMC); Kiswahili, French ,Chinese (KFC); Kiswahili, English, Chinese (KEC); Physical Education, Biology, Fine Art (PBF) na Physical Education, Geography, Economics (PGE).
Jafo amesema tahasusi ya PMC itatolewa katika shule ya sekondari ya Dodoma ambayo itakuwa maalumu kwa wasichana ambapo kwa wavulana itakuwa sekondari ya wavulana ya Iyunga.
Amesema tahasusi ya KFC na KEC itatolewa katika shule ya sekondari ya wasichana Morogoro na ya wavulana Usagara wakati PBF na PGE itatolewa shule ya sekondari ya wasichana ya Makambako, shule ya sekondari ya wavulana Kibiti na sekondari ya Mpwapwa ambayo ni ya mchanganyiko.