Serikali ya nchi ya mali, imetangaza vifo vya raia wake zaidi ya130, vilivyotokea kufuatia shambulio la watu wanaoshukiwa kuwa ni wanamgambo wa Jihad, waliochoma moto nyumba na kufanya utekaji nyara katikati mwa miji ya nchi hiyo.
Maafisa wa usalama katika eneo hilo, wamesema matukio ya mauaji ya kimfumo yaliyofanywa na watu wenye silaha eneo la Diallassagou na miji miwili ya jirani katika mzunguko wa Bankass, unaodaiwa kuwa ni kitovu cha vurugu za wanamgambo.
Rais wa chama cha USR na rafiki wa waathiriwa wa tukio hilo, Nouhoum Togo ambaye anaishi katika mji mkuu wa eneo hilo, alifanikiwa kuepuka mauaji hayo na kusimulia namna mauaji hayo yalivyofanyika kwa kudai watu wao walikuwa wakihoji dini ya muhusika kabla ya kumuua.
“Walikuja, wakawauliza watu kwa lugha ya kabila la wafulani ninyi sio Waislamu?, wakasema tena ninyi sio Waislamu? halafu wakawachukua wale watu kama mia moja hivi wakatoka nao, wakawapiga risasi na wengine wakaondoka nao, siku iliyofuata tukagundua miili iliyokatwa,” alisimulia Togo.
Tangu mwaka wa 2012, Mali imekuwa ikikumbwa na uasi wa makundi yenye uhusiano na Al-Qaeda na kundi linalojiita Islamic State kitu ambacho kimeitumbukiza nchi hiyo katika migogoro.
Hata hivyo, ghasia zilizoanza eneo la kaskazini zimeenea hadi katikati ya Taifa hilo na nchi za jirani za Burkina Faso na Niger, huku ikidaiwa raia wanaouawa mara nyingi hukabiliwa na kisasi na wanajihadi ambao huwashutumu kushirikiana na adui.