Prisca Ulomi na Projestus Binamungu, Mwanza
Serikali imetenga shilingi bilioni 45 za kutekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi nchini kwa kujenga miundombinu ya anwani hizo kwenye halamshauri 194 nchi nzima zilizopo Tanzania Bara na Visiwani.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati akiwa ziarani mkoani Mwanza kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mpango huo kwenye Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikiwa ni eneo la mfano ili kujifunza kwa lengo la kufanikisha utekelezaji huo ili kuzifikia halmashauri zote 194 nchini ambapo halmashauri 184 ni za Tanzania Bara na halmashauri kumi ni za Tanzania Visiwani.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa kila mtaa unakuwa na jina lake na kila nyumba iwe na namba yake, hii inarahisisha utendaji kazi wa Serikali hata ndani ya jamii kwenye shughuli zetu za kiuchumi, tunaongelea kuwa na uchumi wa kidijitali, uchumi wa kidijitali hauwezekani bila kuwa tumekamilisha mfumo huu wa anwani za makazi, tunamshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia shilingi bilioni 45 ndani ya Wizara yangu kwa zoezi hili tu,” amesema Dkt. Kijaji
Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuwafikia wananchi kule walipo ili mwananchi anapopata tatizo, iwe ameunguliwa na moto pale alipo ni rahisi kuwapigia zimamoto na kuwaarifu mtaa na nyumba ulipo, au una mgonjwa unahitaji huduma ya gari ya wagonjwa, unaawarifu wanakufikia na kwa mwananchi aliyeagiza mzigo au kifurushi kutoka nje ya nchi hana sababu ya kwenda posta kufuata mzigo bali mzigo wako utaletwa mpaka ulipo ili wananchi watumie muda wao mwingi kujiletea maendeleo yao.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa kazi hii ya utekelezaji wa anwani za makazi nchini nzima utatekelezwa na wananchi wenyewe waliopo kwenye maeneo hayo na itatoa ajira kwa wananchi hao na ametoa rai kwa wananchi kuwa tayari kujitokeza kutekeleza mpango huu wa anwani za makazi na postikodi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa wananchi wana kiu ya kujulikana kwa kuwa sasa mitaa yao ina majina na nyumba zao zina namba ambapo mwananchi analetewa mzigo wake pale alipo kwa kuwa sasa anatambulika mahali anapoishi.
Diwani wa Nyamagana, Biko Kotecha akizungumza kwa niaba ya wananchi wake ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi kwa kuwa mradi huu una tija kwa wananchi, wananchi wake wamefurahi kwa kuwa mwananchi akipata ajali anaeleza moja kwa moja mahali alipo na anapata huduma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam wa Anwani za Makazi na Postikodi, Hlamashauri ya Jiji la Mwanza ndugu Moses Seleki amesema kuwa jumla ya nyumba 108,000 zimefungwa namba za nyumba, nguzo 5,800 zimewekwa zenye vibao vya majina ya mitaa na nyumba 98,000 zimeingizwa kwenye mfumo wa anwani za makazi wa simu ya mkononi.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari