Serikali imeiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kuandaa miundombinu ya maegesho ya meli kwa ajili ya meli mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” inayojengwa katika Bandari ya Mwanza.
Akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa meli hiyo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema kuwa kazi za ujenzi wa meli hiyo kwa sasa zimefikia asilimia 53.8 na ifikapo mwezi Aprili, 2022 meli hiyo itaingizwa majini kwa mara ya kwanza na kuendelea kumaliziwa ujenzi wake ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2022 na baadae kufanyiwa majaribio ambapo Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) litakagua meli kabla ya kuanza kutoa huduma.
“Meli hii ni kubwa kuliko meli zote zinazofanya safari katika Ziwa Victoria kwani ina urefu wa mita 92.6, upana mita 17 na kimo mita 20, hivyo MSCL kwa kushirikiana na TPA hakikisheni miundombinu ya maegesho kwa ajili ya meli hii inaboreshwa ili meli itakapokuwa tayari iweze kuanza kazi mara moja kwani meli hii ni inatarajia kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma za usafiri wa maji katika Ziwa Victoria,” Amesema Kasekenya
Aidha, Mhandisi Kasekenya amesema kuwa meli hiyo itakapokamilika itafungua fursa za kiuchumi na kibiashara kati ya jiji la wa Mwanza, mikoa jirani ya Musoma, Bukoba kupitia Bandari ya Kemondo Bay pamoja na nchi jirani za Uganda na Kenya.
Kwa Upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Philemon Bagambilana amemueleza Naibu Waziri Kasekenya kuwa ujenzi wa meli ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” unagharimu dola za kimarekani milioni 39 sawa na shilingi Bilioni 89.7 na umeenda sambamba na ujenzi wa chelezo kipya kinachotumika kwenye ujenzi wa meli hiyo ambacho pia kimegharimu dola za Kimarekani milioni15.
Naye, Kaimu Meneja wa Bandari ya Ziwa Victoria, Vicent Steven, amemueleza Naibu Waziri Kasekenya kuwa tayari TPA imeshafanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kupanua na kuboresha miundombinu ya maegesho yote yatakayopokea meli hiyo na kwamba kwa sasa wako kwenye hatua za manunuzi yatakayo wezesha kumpata mkandarasi atakayeifanya kazi hiyo.
Meli mpya ya MV MWANZA “Hapa Kazi Tu” inajengwa na wakandarasi kutoka kampuni ya GAS Entec Company na KANGNAM Corporation za Korea Kusini na itakapokamilika inatarajiwa kuwa na madaraja sita (6) yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200, magari madogo 20, magari makubwa 3 pamoja na mizigo tani 400 na hivyo inatarajiwa kuwa meli kubwa kuliko zote katika Ziwa Victoria.