Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango ameziagiza Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Maji kufanya kazi kwa kushirikiana katika ujenzi wa miradi yake ili pale panapojengwa miradi ya maji kuwe pia na miundombinu ya Zimamoto.

Ametoa maagizo hayo hii leo April 28,2023 wakati wa ufunguzi wa jengo la kituo kikuu cha Zimamoto na Uokoaji wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.

Amesma, miji inazidi kukua, hivyo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji liendelee kubuni mbinu mbalimbali za utendaji kazi.

Pia, ameiagiza wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kushirikiana na viongozi wa mikoa mbalimbali katika kutenga maeneo ya ujenzi wa vituo vya Zimamoto na Uokoaji.

Kwa upande wa Serikali Makamu wa Rais amesema, itaendela kufanya jitihada za kutafuta fedha za kuliwezesha jeshi hilo ili liweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Nae, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema serikali imejipanga kuboresha utendaji kazi na maslahi ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Amesema Serikali inakwenda kulifanya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa la kisasa kwa kuwekeza fedha zaidi ili liwe bora zaidi.

Aidha, Waziri Masauni amesema Serikali itaendelea kujenga vituo vya zimamoto na uokoaji nchini, lengo likiwa ni kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa na jeshi hilo kwa Wananchi.

Awali, akizungumza Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, John Masunda amesema jengo hilo la Kituo Kikuu cha Zimamoto mkoani Dar es Salaam limegharimu Shilingi Bilioni 4.9.

Aidha,  ameishukuru Serikali kwa kuendelea kulisaidia jeshi hilo katika kuboresha maslahi ya Watendaji pamoja na vitendea kazi.

Amesema, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea na ujenzi wa vituo mbalimbali na kutoa mafunzo kwa maafisa wake, ambapo hivi karibuni askari 27 wamepatiwa mafunzo ya uokoaji wa kwenye maji.

GGML yaja na teknolojia za kisasa maonesho ya OSHA
Rais Kagame ahitimisha ziara Tanzania