Serikali imezipa muda wa miezi sita taasisi zote za fedha na benki mbalimbali nchini ambazo zimeendelea kutoza riba kubwa kwa wafanyabiashara wanaochukua mikopo kwao, kuhakikisha wanapunguza riba kama ambavyo imekuwa ikielekeza.
Imebainisha kuwa endapo taasisi hizo na benki zitashindwa kushusha riba hizo, itaingilia kati suala hilo kwa kutoa maagizo ya kisheria kwani imewapatia muda wa kutosha kuhakikisha wanashusha wenyewe.
Kauli hiyo imetolewa na naibu waziri wa Fedha, Ashatu Kijaji wakati akizungumza na wanayabiashara na wawekezaji wa mkoa wa Simiyu kwenye mkutano wa majadiliano uliolenga kutatua changamoto zinazowakabili.
Amesema Serikali ilichukua hatua kubwa ya kuzipunguzia riba kupitia benki kuu ya Tanzania (BoT), taasisi hizo na benki zinazotoa mikopo kutoka asilimia 16 hadi 7.
Kikaji amesema lengo la Serikali kupunguza riba hiyo ni kuziwezesha taasisi hizo na benki na wao wapunguze riba kwa wateja wao ambao wengi ni wafanyabiashara lakini bado wameshindwa kufanya hivyo.
” Serikali kila mara tunaelekeza hizi benki na taasisi kupunguza lakini tunaona bado zimeendelea kutoza riba hadi asilimia 18, kama Serikali tumefanya upande wetu tanawashangaa wao wameshindwa nini” Amesema Kijaji.
Katika hatua nyingine, Kijaji amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuzitafuta taasisi ndogo za kifedha ambazo zinawakopesha wananchi wakiwemo walimu kwa riba kubwa na masharti magumu.