Serikali nchini, imewataka maafisa ununuzi na ugavi kuzingatia ukomo wa matumizi ya kemikali na vifaa vyenye kemikali ambazo zinamong’onyoa tabaka la ozoni au kuwa na athari kwa afya ya binadamu na mazingira.

Hayo yamebainishwa hii leo Agosti 25, 2023 Jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Switbert Mkama wakati akifungua warsha ya mafunzo kwa Maafisa ununuzi na ugavi kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Montreal inayohusu kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni.

Amesema, mwanzoni mwa miaka ya 1970, wanasayansi walibaini baadhi ya kemikali zinazotengenezwa na binadamu ikiwemo majokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto na utengenezaji wa magodoro vimejipenyeza angani na kumong’onyoa tabaka la hewa ya Ozoni na kusababisha madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Switbert Mkama (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa ununuzi na ugavi muda mfupi baada ya kufungua warsha kuhusu utekelezaji wa itifaki ya montreal inayohusu Kemikali zinazomong’onyoa tabaka la Ozoni katika ukumbi wa Mikutano wa St. Gaspar Jijini Dodoma leo Ijumaa (Agosti 25, 2023).

“Matokeo ya kumong’onyoka kwa Tabaka la Ozoni ni kuruhusu mionzi zaidi ya urujuani kufikia uso wa dunia ambayo husababisha madhara mbalimbali kwa afya ya binadamu na mazingira. Madhara hayo ni kama vile saratani ya ngozi, uharibifu wa macho unaosababisha upofu na athari kwa kwa ukuaji wa mimea na viumbe hai wengine,” amesema Dkt. Mkama

Aidha, Dkt. Mkama amesema matokeo ya uvumbuzi huo yalisababisha Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Mazingira (UN Environment) kufanya tathmini ya kisayansi na kuamua kuchukua hatua madhubuti kulinda tabaka la Ozoni kwa kuanzisha Itifaki ya Montreal kuhusu udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni iliyopitishwa mwaka 1987.

COSTECH kutoa usaidizi kwa vituo vya ubunifu
Phiri, Baleke waandaliwa mkakati maalum