Serikali ya awamu ya tano kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Watu wenye ulemavu imesema haioni haja ya kufuta tozo ya kuvukia daraja la Kigamboni kwa watembea kwa miguu na vyombo vya moto ili wapite bure kwasababu daraja hilo limefanyiwa uwekezaji na linatakiwa kukusanya pato.
“Ninaomba ieleweke kwamba daraja la Kigamboni ni sehemu ya uwekezaji la Shirika la Taifa Hifadhi ya Jamii (NSSF), na fedha iliyotumika kwaajili ya uwekezaji huo ni fedha ya wanachama ambapo mwishoni pia fedha hiyo hiyo huwa inatumika kwenda kulipia mafao ya watu. Hivyo hatuwezi katika hali ya kawaida kufuta tozo na watu wakapita bure katika eneo hilo kwasababu ni eneo la uwekezaji”, amesema Antony Mavunde.
Hayo yamesemwa leo Juni 22, 2018 Bungeni Jijii Dodoma, na Anthon Mavunde wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa viti maalum Zainab Mndolwa Amiri aliyetaka kufahamu ni lini serikali itasitisha tozo katika daraja la kigamboni kwa kuwa madaraja yote watu hupita bure.
Aidha, Mavunde amesema Serikali kupitia shirika la taifa hifadhi ya jamii NSSF.99 ambao ndio wanasimamia uendeshaji wa daraja hilo hadi kufikia mwezi Machi 2018 limeshakusanya kiasi cha takribani shilingi Bilioni 19.7 tangu daraja hilo lilipoanza kutumika rasmi mwezi Mei mwaka 2016.