Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa suala la tozo za miamala ya simu limeanza kufanyiwa kazi na kwamba taratibu zinakamilishwa na hadi kufikia mwisho wa mwezi Julai serikali itatoa majibu juu ya suala hilo.
Amesema hayo kupitia ukurasa wa mtandao wa Twitter wa Msemaji Mkuu wa Serikali, zikiwa zimepita siku kadhaa tu tangu Rais Samia Suluhu Hassan, atoe maelekezo kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, kuhakikisha wanashughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu tozo za miamala.
Tozo ya uzalendo katika miamala ya simu kwa mtumaji ama mpokeaji wa pesa zilianza kutozwa Julai 15 mwaka huu, ambapo kufuatia hatua hiyo wananchi walianza kulalamika kwani makato ni makubwa ikilinganishwa na yale ya awali yaliyokuwa yamezoeleka.