Serikali imetoa ufafanuzi juu ya marekebisho ya Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana na kubainisha kuwa masharti ya mikopo ya nje, yaliyowekwa dhidi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), yanatokana na masharti ya wadau wanaotoa mikopo hiyo.
Aidha, imebainisha kuwa kupitia marekebisho hayo ya Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana inayopendekeza na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufaulisha mkopo kwa SMZ, yana nia njema na yamelenga kuwahakikishia wahisani hao kuwa masharti yao yanafuatwa.
Hoja hiyo iliibuka baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 4 wa Mwaka 2016 bungeni mjini Dodoma jana.
Aidha, ufafanuzi huo umetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, ambapo ametaja baadhi ya wadau wanaoikopesha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Saudi Fund, kuwa katika moja ya sehemu ya makubaliano ya primary loans wanahitaji kuona kuna utaratibu wa wanaonufaika kuwajibika katika malipo.
“Haya si masharti ya SMT ni masharti ya wanaotukopesha, mkiyafungia mtawekewa vikwazo kwa hawa wanaotukopesha kwa masharti nafuu,” amesema Dkt Mpango.
Vilevile Amesema lengo la muswada huo, ni kuweka kisheria kwamba fedha zinazokopeshwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa SMZ zinawasilishwa kwa masharti yaliyopo na zinalipwa kama ilivyopangwa lakini pia kuhakikishia wahisani hao kuwa masharti waliyoweka ya ukopeshaji yanafuatwa.