Serikali imekanusha taarifa zilizokuwa zimesambaa zikieleza kuwa imemfukuza Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini,
Reoland van de Geer kwa kumpa saa 24 tangu jana.
Akizungumza leo na vyombo vya habari jijini Arusha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agustine Mahiga amesema kuwa balozi huyo hajafukuzwa bali ameitwa na waajiri wake waliomtuma.
“Ameitwa na Shirika lake la Umoja wa Ulaya, na mara nyingi kitu kama hicho kuwa kinatokea. Mtu anaitwa na Serikali yake anapewa majukumu mengine. Lakini kwa sababu tumekuwa tunafanya nao kazi vizuri kwa miaka mingi, tunashauriana na tunapewa taarifa kwamba huyu mtu anaondoka… na sisi tunaafiki,” alisema Balozi Mahiga.
“Hata mimi nilipokuwa Balozi, mara kwa mara nilikuwa naitwa nyumbani wanasema ‘uje tushauriane, tuzungumze na utupe muelekeo’. Ni kueleza na kutoa taarifa kwa wale waliokutuma yale yanayojili huko walikokutuma,” aliongeza.
Aidha, Balozi Mahiga alisema kuwa uamuzi juu ya Balozi huyo wa Umoja wa Ulaya nchini kurejea au kupangiwa kazi nyingine uko mikononi mwa Shirika hilo lililomtuma na sio vinginevyo.
Jana, Afisa Habari wa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya Nchini, Sussanne Mbise alisema kuwa hawana taarifa kuhusu kufukuzwa kwa Balozi. Alisema kuwa wanachofahamu ni kwamba Balozi huyo ameitwa makao makuu ya Umoja wa Ulaya kwa ajili ya mazungumzo.