Serikali imetoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kuunga mkono jitihada za ukarabati na ujenzi kituo cha kitalii Wilayani Kongwa Jijini Dodoma ambacho kitahifadhi kumbukumbu za Baba wa Taifa Hayati Mwl.Julius Nyerere .
Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alipokuwa akijibu Swali la Msingi la Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) lililokuwa likiuliza ni lini serikali itajenga maktaba yenye kumbukumbu za kazi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo kituo hicho kitakuwa sehemu ya utalii na kitajengwa Makao Makuu ya nchi Jijini Dodoma.
“Katika utekelezaji wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, Serikali imeteua Wilaya ya Kongwa kuwa Kituo Kikuu cha Kumbukumbu za ukombozi nchini na katika kituo hicho kitakuwa na miundombinu kadhaa ya uhifadhi wa historia za viongozi ambazo zitajengwa ikiwemo kazi adhimu za Baba wa Taifa,”amesema Shonza.
Aidha, amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na UNESCO imekarabati Studio za Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) zilizopo Barabara ya Nyerere na kuwa kituo adhimu cha hifadhi rejea ya kazi za Baba wa Taifa.
Pamoja na hayo, Shonza amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho cha kumbukumbu cha Kongwa umekwishaanza tangu mwaka 2015 ambapo ukarabati wa kituo hicho ulikwisha anza na unaendelea na pia kuna mipango mikubwa katika kituo hicho ikiwemo kujenga miundombinu ya kisasa mfano hoteli za nyota tano na kiwanja cha ndege.
-
Video: Pinda azindua kinywaji cha Kweichow Moutai
-
Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa yateketeza Nyavu na Mitumbwi Bandia
-
Video: Askofu Shoo amaliza utata, atumia msiba wa Mengi kuonya viongozi na matajiri
Hata hivyo, ameongeza kuwa serikali inaunga mkono juhudi za taasisi mbalimbali zinazofanya uhifadhi wa amali za Urithi wa kumbukumbu za Baba wa Taifa na baadhi ya taasisi hizo ni Maktaba ya Taifa Dar es Salaam, Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam, Makumbusho ya Mwl. Nyerere Butiama, Taasisi ya Mwalimu Nyerere na Vituo vya Televisheni vya TBC na ITV.