Waziri wa sheria wa Taliban, Abdul Hakim Sharaee wa Afghanistan, ametangaza kupigwa marufuku kwa Vyama vyote vya Kisiasa nchini humo akisema kuwa ni kinyume cha sheria za kiislamu au Shariah kwa mujibu wa imani yao.
Hatua hiyo, imefikiwa baada ya viongozi waliochukua madaraka ya Afghanistan kuadhimisha mwaka wa pili wa tangu kurejesha utawala wao mjini Kabul na limetolewa wakati akihutubia Wanahabari mjini Kabul.
Katika nchi hiyo, zaidi ya vyama 70 vya kisiasa vilikuwa vimesajiliwa rasmi na Wizara ya Sheria, hadi pale Taliban ilipochukua udhibiti wa taifa hilo lililokumbwa na mapigano miaka miwili iliyopita.
Tangu wakati huo, utawala huo umekuwa ukilaumiwa kuminya uhuru wa kutangamana, kukusanyika na kujieleza, ikiwa ni mbinu mojawapo ya kuwanyamazisha wakosoaji, huku wafuasi wake wakiruhusiwa kuendesha shughuli zao kama kawaida.
Sheria kali za kiislamu zimewekwa kwenye taifa hilo la Kusini mwa Asia, zikiwemo za kupiga marufuku Wasichana kuhudhuria masomo, pamoja na kuzuia wanawake wa Afghanistan kufanya kazi au kujitokeza mbele ya umma.