Serikali imepata kodi ya Shil mil. 466.4 kutokana na mauzo ya Sh9.3 bilioni ya madini ya Tanzanite kupitia mnada uliofanyika mjini Arusha.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uthaminishaji wa Almasi na Vito kutoka Wizara ya Nishati na Madini (Tansolt), Archard Karugendo, amesema katika mauzo hayo Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imepata Sh27.9 milioni.
Amesema kuwa katika mnada huo wa pili kufanyika nchini, Kampuni ya TanzaniteOne inayomilikiwa kwa ubia kati ya Sky Associate na Stamico, ndiyo iliongoza kwa kuuza madini na kupata Sh8.8 bilioni.
Aidha,kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendela amesema licha ya madini hayo kuwa ni ya Taifa, ni muhimu wakazi wa Wilaya ya Simanjiro waone matunda yake.
Ameongeza kuwa ni aibu Tanzanite inatoka Simanjiro, lakini wilaya hiyo ndiyo ya mwisho kwa elimu Mkoani Manyara na kuwapo kwa shida kubwa ya maji, huduma za afya na Mererani inaongoza kwa maambukizi ya HIV ambayo yamefikia asilimia 18.
Hata hivyo kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe amesema wizara hiyo, itaendelea kuwezesha minada ili kuhakikisha wanunuzi wakubwa wa madini wanafika nchini kununua madini katika masoko yanayotambulika kisheria.