Serikali Nchini, imesema itaendelea kupambana ili kuwatoa Watanzania katika lindi la umasikini na kwamba pia itaendelea kulinda uhuru wa Wananchi wa kutoa mawazo, kuwa na imani na uhuru wa kuabudu na kwamba itahakikisha kunakuwa na amani na utulivu kwa ustawi wa maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo, imetolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Biteko alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za kumpongeza Mhasham Askofu Mkuu Mstaafu, Paul Ruzoka na kumpokea rasmi Askofu Mkuu Mpya wa Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, zilizofanyika Jimbo Kuu, Kanisa Katoliki Tabora.
Amesema, “Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan muda wote amekuwa akisisitiza haki kwa wananchi wote, na ili kuishi katika misingi ya utangamano, haki lazima itawale, tunaweza kutofautiana katika maoni na mitazamo lakini kamwe tusivunje umoja wa kitaifa, tuwaunganishe watanzania na tupambane kuwaondoa wananchi katika umaskini na kuwaletea nafuu kubwa ya maisha.”
Dkt. Biteko amesema Serikali imeweka msisitizo katika kupeleka maendeleo kwa wananchi wote bila kuangalia tofauti zao, ikiwemo maji, Barabara, umeme, shule na pia inalenga kuendelea kuwaunganisha wananchi, ili kuleta umoja nchini na kwamba Rais Dkt. Samia yupo tayari kushirikiana na taasisi za kidini katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Kwa upande wa Askofu Mpya wa Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa na Mhasham Askofu Mkuu Mstaafu Paul R. Ruzoka wameshukuru kwa ushirikiano ambao Serikali imeendelea kuwapatia na wameahidi kuwa pamoja.