Serikali imetoa onyo kali kwa mtu yeyote mwenye nia ya kuhujumu Miradi ya Serikali kwa maslahi binafsi kuacha mara moja na endapo atathibitika kuhusika na suala hilo sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.

Hayo yamesemwa mkoani Morogoro na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni wakati alipotembelea Kiwanda na Shamba la Miwa katika Gereza la Mbigiri ambalo linakadiriwa kuzalisha tani za sukari laki mbili kwa Mwaka na kuondoa adha ya kuagiza sukari nje ya nchi.

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kukuza viwanda mbalimbali ikiwemo kiwanda cha Sukari Mbigiri na kuwezesha mamia ya wananchi kupata ajira pamoja na kukuza uchumi wa nchi.

“Kuna taarifa za baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa sukari kupenyeza maslahi yao binafsi katika miradi hii mikubwa ya serikali ikiwemo shamba hili la miwa hapa Mbigiri, nawaasa waache mara moja kwani watakapobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa juu yao ikiwemo na kosa la uhujumu uchumi,” amesema Masauni

Akitoa taarifa ya shamba hilo Mkuu wa Gereza Mbigiri, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Shija Fungwe amesema kuwa shughuli zinaendelea katika shamba hilo kwa kutumia nguvu kazi ya wafungwa kutoka katika gereza hilo huku wafungwa 280 wakitumika katika shamba hilo.

Hata hivyo, ameongeza kuwa kazi ya kupanda eneo lililo tayari inaendelea huku kazi ya kulima hekta 500 inaendelea na kati ya hizo hekta 200 zimeshalimwa kwa awali na lengo lao kufikia mwezi juni mwaka huu inatakiwa zilimwe hekta 700 wakitumia nguvu kazi ya wafungwa.

 

Serikali yajipanga kutangaza Utalii kupitia mashindano ya AFCON U17
Wabunge wasusa watoka nje kupinga adhabu ya Halima Mdee