Serikali imesema kuwa haitasita kuwachukulia hatua watu wanao wanyanyasa watoto kwa kukiuka Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009.
Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Josephat Kandege alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mgebi Jadi Kadika juu ya mikakati ya Serikali ya kuondoa tatizo la kuwakosesha watoto haki za msingi na malezi bora kwa kuwatumia katika kutoa huduma ya kubeba mizigo na kupewa ujira mdogo.
”Huduma za ulinzi wa mtoto zinatekelezwa kupitia Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009. Katika kusimamia utekelezaji wa Sheria hiyo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa Fedha 2017/18 hadi 2021/22,” amesema Kandege.
Amesema kuwa, tathmini imebaini kuwa watoto wengi wanaojihusisha na kazi za kubeba mizigo masokoni ni matokeo ya umaskini uliokithiri kwa baadhi ya Kaya, kuondokewa na wazazi wao kwa maambukizi ya UKIMWI, migogoro ya ndoa na ukatili dhidi ya watoto.
Aidha, amesema kuwa mkakati unaotekelezwa na Serikali ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za msingi za mtoto kupata elimu na malezi bora, ambapo utoaji wa elimu ya msingi bila malipo umetoa fursa kwa watoto wengi wenye umri wa kwenda shule kuandikishwa kuanza elimu ya awali kupitia mfumo rasmi na mfumo usio rasmi.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wazazi kutimiza wajibu wao wa kuwalea, kuwatunza na kuwalinda watoto ambao ni Taifa la kesho kwa kutowatumikisha katika kazi ambazo haziendani na umri wao.