Utekelezaji wa Mpango wa Malezi na Makuzi kwenye vituo vya kijamii – ECD Centers, unaokwenda kujengwa nchi nzima, unatarajia kuwanufaisha wazazi kwa kuwapatia elimu kuhusu malezi ya watoto.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifungua mafunzo ya wakufunzi wa watoa huduma ya malezi kwa watoto, Mkoani Morogoro.
Amesema, “asilimia 53 ya watoto Tanzania, haiko kwenye mfumo mzuri wa kuweza kupata yale wanayotakiwa kuyapata kama watoto ili wakue vizuri, hapa nazungumzia changamoto za mmomonyoko wa maadili, afya, lishe na elimu.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto Sebastian Kitiku, amesema uwepo wa changamoto ya wazazi kuwa na msongo wa mawazo unapelekea changamoto za afya ya akili zinazowasukuma kuwafanyia ukatili watoto wao, hivyo programu ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto itasaidia kutimiza malengo ya Serikali.
Mafunzo hayo, yameandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani – UNICEF, kwa kuwaleta pamoja wataalamu kutoka Serikalini na Sekta Binafsi.