Serikali imewasahuri wananchi wote wanaofaidika na Mpango wa kunusuru Kaya Maskini (TASAF) nchini kuzitumia vizuri ruzuku wanazozipata kwa kuendelea kujishughulisha na shughuli za kiuchumi katika maeneo yao.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtabwe, Khalifa Mohamed Issa aliliouliza kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kama upo katika Awamu ya Tatu ya Utekelezaji wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini nini kimefanyika ili ruzuku ziweze kumudu mahitaji ya chakula, Elimu, Afya na lishe Bora kwa watoto.
Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa ruzuku wa Kaya Maskini ila inashauri pia wananchi waendelee kujishughulisha na kazi nyingine za kuongeza kipato na isitegemee ruzuku pekee.
“Niwaombe wananchi wanaopata ruzuku kutoka mpango wa TASAF wajishughulishe pia na shughuli nyingine za kiuchumi na kutotegemea ruzuku pekee” Amesema Angella Kairuki.
Ameongeza kuwa ruzuku zinazotolewa ni kichocheo cha kuifanya kaya iweze kujikimu hasa katika kupata mahitaji muhimu huku ikiendelea kujiimarisha kiuchumi kwa kuweka akiba na kutekeleza miradi ya ujasiriamali ili iweze kusimama yenyewe na kujitegemea baada ya kutoka katika umaskini uliokithiri.
Aidha, Angellah Kairuki amesema kuwa vigezo vya kupata kaya maskini ni wa uwazi na huanishwa na Jamii katika mkutano wa hadhara unaoendeshwa na wawezeshaji kutoka Halmashauri za Wilaya na kusimamiwa na Viongozi wa Vijiji, Mitaa na Shehia.
Hata hivyo, amesema kuwa uzoefu uliopatikana umeonesha kuwa kwa kiwango cha ruzuku kinachotolewa kwa wananchi wanaofaidika na Mpango huo kimewawezesha kuboresha maisha yao kwa kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo ufugaji,ujasiriamali na ujenzi wa nyumba bora, hivyo viwango hivyo sio vidogo kama wengi wanavyodhani