Serikali kupitia Wakala wa Misitu Tanzania imewataka watendaji kuanzia ngazi ya kijiji kupanda miti takribani kiasi cha hekta 185,000 za miti kwa mwaka ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa misitu nchini.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi ya Rasilimali, Wakala wa Misitu Tanzania  Bw. Mohamed Kilongo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utaratibu wa uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu.

Alisema kuwa ifikapo mwaka 2030 upungufu wa misitu utakuwepo  endapo serikali haitatekeleza mkakati wa upandaji wa miti, hivyo kuwataka watendaji hao kutekeleza mkakati wa upandaji wa miti uliowekwa na Wakala wa misitu.

“Tumekubaliana katika mkakati wa kitaifa kuwa kila wilaya kupanda miti Milioni 1.5 kila mwaka ili kuondokana na tatizo la upungufu wa misitu nchini ifikapo mwaka 2030” Alifafanua Bw. Kilongo.

Aliongeza kuwa upungufu huo unatokana na kichocheo cha uvunaji haramu na holela ndani ya misitu ya hifadhi, mapori ya akiba na hata ndani ya hifadhi za taifa hivyo kuwataka wavunaji wa mazao ya misitu kufuata sheria na taratibu zilizopo.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa huduma za Misitu Prof. Dos Santos Silayo alisema kuwa endapo wavunaji na wasafirishaji  wa mazao ya misitu watatumia taratibu za uvunaji na usafirishaji wa mazao hayo itasaidia kuongeza pato la taifa.

“Vyombo vyote vitakavyohusika na kusafirisha mazao ya misitu ni lazima viwe wazi ili ukaguzi ufanyike kwa urahisi na ufanisi ambapo kila atakayesafirisha mazao ya misitu anapaswa kusimama kwenye kizuia kwa ajili ya ukaguzi”alisema Prof Silayo.

Mbali na hayo Wakala wa Misitu Tanzania imejipanga kutoa mafunzo maalumu kwa wananchi juu ya uhifadhi, uvunaji,usafirishaji, usimamizi na utunzaji wa mazao ya Misitu

Museveni awataka wapinzani wake kushika nyaya zenye umeme
Ummy Mwalimu Amuaga Mwakilishi Wa Shirika La Umoja Wa Mataifa UNFPA