Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Wizara ya Nishati inafanya jitihada mbalimbali ili kupunguza makali ya umeme nchini na hivyo kuwaondolea wananchi matatizo ya umeme wanayoyapata kwa sasa.
Biteko ameyasema hayo hii leo Oktoba 2, 2023 baada ya kuwasha umeme katika Kijiji cha Nyanguku na Bunegezi wilayani Geita, Mkoa wa Geita ambapo pia alizungumza na wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya maji na barabara katika vijiji hivyo.
Amesema, “Tumekubaliana, Katibu Mkuu na Watendaji Wakuu wa Taasisi warudi Dodoma kushughulikia masuala ya mgawo wa umeme, tunataka tupunguze mgao huu kwa kasi kubwa ili wananchi wasipate matatizo ya umeme.”
Aidha ameongeza kuwa, Wizara ya Nishati inalitekeleza agizo la Rais Dkt. Samia la kushughulikia changamoto za upatikanaji umeme wa uhakika ndani ya miezi sita, ili Wananchi waweze kufanya shughuli za kiuchumi.