Serikali imesema inaandaa mpango mkakati maalum wa kusaidia kukomesha mauaji ya watu mbalimbali yanayoendelea nchini.
Kauli hiyo ya Serikali imekuja wakati kukiwa na matukio ya watu kuuliwa kikatili maeneo mbalimbali.
Haya yamesemwa leo Alhamisi Februari 3, 2022 Bungeni na Waziri wa Maendeleo ya Jamii Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Iringa, Jeska Msambatavangu.
Msambatavangu aliuliza swali la nyongeza akitaka kujua mkakati wa Serikali kukomesha mauaji.
Dk Gwajima amesema tayari wameanza kupeleka muongozo kwa viongozi wa Vijiji kwa kutoa elimu na kuwekeana mkakati maalumu.
Waziri amesema wataitumia Februari 6, ambayo ni siku ya kupinga ukeketaji ili kuzungumza na wananchi na kupeana mbinu za kumaliza mauaji hayo.