Mashirika ya UMMA yanayojiendesha kwa hasara Nchini yametakiwa kuanza kujitathmini Katika uendeshaji wake.
Hayo yamesemwa na Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alipokuwa akizungumza Katika kikao kazi na Wahariri wa Vyombo vya Habari chenye lengo la kupitia mpango kazi wa mageuzi yenye tija kwenye Taasisi za Umma kwa maendeleo ya Taifa na kuangazia muswada wa sheria ya mamalaka ya uwekezaji wa UMMA na Wanahabari Novemba 28, 2023.
Mchechu amefafanua kuwa, mapema wiki ijayo ofisi yake itatolea ufafanuzi wa kuyapunguza Mashirika 19 yanayojiendesha kwa hasara ili kuiondolea mzigo Serikali kwa kuwa na utitiri wa Mashirika yasiyo na tija.
Katika hatua nyingine ameeleza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya uwekezaji wa shilingi trillioni 73 katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala wa Serikali 298 ambazo zinafanya shughuli mbalimbali, huku asilimia 86 za taasisi hizo zikitoa huduma za kijamii.
Imeelezwa kuwa kutokana na mipango na mikakati iliyopo baada ya miaka mitano baadhi mashariki yanakwenda kufanya vizuri, huku watendaji wa mashirika hayo watapimwa kutokana ufanisi wa kazi katika kuhakikisha wanafikia malengo kutokana uwekezaji mkubwa unaoendelea kuwekwa ikiwemo wa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo mashirika 108 yalipata mapato ya shilingi bilioni 777.
Mnamo mwaka 2021/2022 mashirika 136 yalipata mapato ya shilingi bilioni 645 na mwaka 2020/2021 mashirika 200 yamepata bilioni 477, huku mwaka 2019/2020 mashirika 236 yameingiza mapato ya bilioni 696.
“Lengo ni kuhakikisha mashirika ya umma yanafanya kazi kwa ufanisi na kuleta faida kwa serikali katika kuhakikisha yanasonga mbele” amesema Mchechu.
Mchechu amesema kuwa wakati umefika kwa wakurugenzi wa mashirika ya umma kufanya kazi wa uweledi katika kuhakikisha wanapata mafanikio katika utendaji wao.
“Ili mashirika ya umma yapige hatua yanapaswa kutoingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yake, kuwekeza rasilimali fedha katika kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuwekeana malengo na wasimamizi katika kufikia viwango vya mafanikio ndani ya muda fulani” amesema Bw. Mchechu.
Amesema kuwa mipango iliyopo kutakuwa na utaratibu wa kuishirikisha Mamlaka kwenye mchakato wa kuwapata wenyeviti, wajumbe wa Bodi na watendaji wakuu wa taasisi jambo ambalo itasaidia katika ufanisi wa kazi.
Mchechu amesema kuwa taasisi za umma zinapaswa kuwekewa mifumo rafiki ambayo itasaidia kutengeneza mapato na kuleta tija kwa Taifa.
Bw. Mchechu amesema kuwa ili kufikia malengo wamependekeza mambo muhimu ya kuzingatia ikiwemo kuanzisha Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (PIA) kwa kubadilisha jina la ofisi ya Msajili kuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (Public Investment Authority- PIA) ili kuakisi majukumu na mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa duniani.
Amesema kuwa kuanzishwa kwa mfuko wa serikali kwa kufanya uwekezaji wa kimkakati itasaidia kuongeza ufanisi wa uendeshaji, kuokoa mashiriki ambayo bila mfuko huo yanaweza kuanguka pamoja na kuwezesha mashirika ya umma kustahimili ushindani.
“Kuainisha vyanzo vya fedha za mfuko wa uwekezaji wa umma ambapo vyanzo vya fedha za mfuko vitakuwa ni pamoja na sehemu ya maduhuli yatakayokusanya na mamlaka ambayo kiwango chake kitabainishwa kwenye kanuni” amesema Mchechu.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deogratius Balile, ametoa pongezi kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuwafanya kazi kwa ufanisi huku akieleza kuwa vyombo vya habari vitaendelea kutoa ushirikiano katika masuala mbalimbali ya maendeleo.