Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezitaka shule zote zilizowataka wazazi/walezi kuwahamisha watoto wao kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu, kufuta agizo hilo na kuendelea na wanafunzi bila masharti yeyote.
Aidha katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamishna wa Elimu, Nicolas Bubeta, imeeleza kuwa wazazi wenye watoto waliorudishwa nyumbani kwa sababu hiyo wahakikishe wanawarudisha kwenye shule walizokuwa wanasoma ili waendelee na masomo kama kawaida.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali imefikia uamuzi huo baada ya kubainika kuwa bado kuna shule nyingi za msingi na sekondari hususani zisizo za serikali na zaidi za kidini zinazo endelea kukaririsha, kuhamishia shule nyingine au kuwafukuza wanafunzi kwa kigezo cha kutofikia alama za ufaulu zilizowekwa na shule hizo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Hata hivyo taarifa hiyo imeagiza wadhibiti ubora wa elimu, kanda na wilaya, maofisa elimu wa mikoa na wilaya kusimamia utekelezaji wa agizo hilo katika maeneo yao.
“Shule yeyote itakayokiuka maagizo hayo itachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria zilizopo,”