Makanisa 714 na msikiti mmoja yamefungiwa na Serikali ya Rwanda huko mjini Kigali kwa kutokidhi masharti yaliyowekwa na Serikali hiyo.
Afisa wa Serikali Justus Kangwagye amesema Serikali imechukua hatua hiyo kwa sababu za kiusalama na kuzingatia usafi wa jiji hilo.
Ambapo baadhi ya makanisa hayo yamekuwa yakifanya kazi bila kuwa na kibali cha leseni ya uendeshaji shughuli hiyo huku mengine yakiwa yanafanya ibada kwa kutumia mahema na hayana maeneo ya kutosha kuegesha magari ya waumini.
Hali iliyopelekea baadhi ya waumini kuegesha magari yao pembezoni mwa barabara na kusababisha msongamano wa magari.
”Shughuli ya kuabudu inafaa kufanywa kwa utaratibu na kwa kutimiza masharti ya viwango vya ubora na usalama vilivyowekwa. Kutumia uhuru wako wa kuabudu hakufai kuingilia haki za watu wengine. Wametakiwa kusitisha shughuli zote hadi watimize masharti yaliyowekwa,” amesema Justus.
Wakazi wa Kigali baadhi wameiunga mkono Serikali kwa hatua iliyochukuliwa dhidi ya makanisa hayo lakini wengine wangependa wenye makanisa hayo wapewe muda zaidi wa kutimiza masharti hayo.
Aidha, Askofu Innocent Nzeyimana, rais wa Baraza la Makanisa katika wilaya ya Nyarugenge ameiomba serikali, kwa niaba ya makanisa, kuyaruhusu makanisa yaliyofungwa yaendelee kuhudumu yanapoendelea kufanya juhudi za kutimiza masharti yaliyowekwa.