Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezionya shule zisizo za serikali zinazofukuza au kuwahamisha wanafunzi kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu ambao shule hizo zimejiwekea bila kufuata wastani uliowekwa na serikali.
Shule hizo zimetakiwa kuacha kufanya hivyo mara moja, na shule itakayokaidi itachukuliwa hatua za kisheria kwa kufutiwa leseni ya usajili au kufungiwa.
Aidha, wizara hiyo pia imewataka wazazi ambao watoto wao walikutana na adha hiyo kuwarejesha katika shule hizo ifikapo Januari 20, 2018.
Hata hivyo, Wanafunzi ambao wamedaiwa kukutana na sakata hilo ni pamoja na wale wanaofanya mitihani ya darasa la Nne na Kidato cha pili ambao hurudishwa darasa au kidato ilihali wakiwa wamefikisha wastani wa serikali.