Serikali nchini Uganda, imeweka vizuizi vya kusafiri katika wilaya mbili zilizokumbwa na virusi vya Ebola ikiwa ni njia mojawapo ya kukomesha kuenea kwa ugonjwa huo wa kuambukiza huku wakazi wa eneo wakidai kutengwa.
Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni alitangaza uamuzi huo utakaowafanya wakazi wa Wilaya za Kati za Uganda za Mubende na Kassanda kutoweza kusafiri ndani au nje ya maeneo hayo kwa njia binafsi au za umma.
Hata hivyo, magari ya mizigo na mengine yanayopita kutoka Kampala kuelekea kusini magharibi mwa Uganda yataendelea na kuruhusiwa kufanya usafirishaji.
Maeneo yote ya burudani, ikiwa ni pamoja na baa, maeneo ya ibada yameamriwa kufungwa na mazishi ya mtu yeyote katika wilaya hizo sasa yanalazimika kusimamiwa na maafisa wa afya.
Museveni pia, ameweka amri ya kutotoka nje usiku, na hali hiyo itaendelea kwa takribani siku 21, huku Rais huyo akidai kuwa hatua hizo ni za muda zikilenga kudhibiti kuenea kwa Ebola.