Saa chache baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa wabunge 17 wa Bunge la Kenya wamepimwa na kukutwa na virusi vipya vya corona (covid-19), Wizara ya afya imesema bado haijapata taarifa rasmi kuhusu ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wabunge hao 17 wamelazimika kutengwa katika eneo maalum na kupatiwa huduma za matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Nairobi, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Mercy Mwangangi amesema, “Wizara inafahamu, na tumeona kwenye vichwa vya habari ripoti kuwa kuna visa vya corona ndani ya Bunge. Lakini hadi wakati huu, bado hatujapokea ripoti rasmi ya taarifa hiyo.”
Wakati huohuo, Mtaalam wa afya kupitia maabara ya Lancet Kenya ambaye alipewa kazi ya kuwapima wabunge kujua hali zao dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, amekanusha taarifa hizo zinazodai wabunge 17 wamekutwa na covid-19.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, maabara hiyo imeeleza kuwa taarifa zote ambazo zinadai kuna visa vya covid-19 ndani ya bunge sio sahihi, zinapotosha na zinapaswa kupuuzwa.
“Taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari kuhusu kuthibitika kwa visa vya corona ndani ya Bunge sio sahihi, zinapotosha na zinapaswa kupuuzwa,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ambayo imenukuliwa na Citizen TV.