Serikali imesema hakuna ubaya kwa wananchi kuchangishwa fedha za kulipia vibao vya anuani za makazi katika maeneo yao.
Kauli hiyo ya serikali imekuja baada ya kuibuka malalamiko katika baadhi ya maeneo ambayo zoezi la anuani za makazi limefanyika ambapo kumedaiwa kufanyika utapeli wa kuwachangisha wananchi kiasi kikubwa cha fedha kwaajili ya vibao hivyo.
Msemaji Mkuu wa serikali Gerson Msigwa amesema kwa mujibu wa kanuni ya 25 na 26 ya anuani za makazi, mwananchi ana wajibu wa kuchangia zoezi hilo kwa mujibu wa makubaliano yatakayofikiwa kwenye vikao vyao.
“Kuchangia si dhambi ila kiasi gani unapaswa kuchangia hilo ndo lenye utata. Kuna baadhi ya maeneo wananchi hukaa kwenye mikutano ya kata au kijiji na kukubaliana kiwango cha kuchangia kulingana na aina ya vibao vya anuani wanavyovihitaji, vingine vya bei rahisi utakuta wanachangishana fedha kidogo kila kaya ila utakuta maeneo mengine wanachagua vibao vya kisasa vyenye miundo ya kuvutia zaidi ambavyo gharama yake ni kubwa,” amesema.
Aidha ameongeza “Ila wanakubaliana na kuvipitisha kisha wanajipangia kiwango cha kuchangishana wao wenyewe. Tumegundua asilimia kubwa ya wanaolalamika kuhusu viwango hivyo ni wale ambao hawahudhurii mikutano hiyo,” amesema Msigwa .
Kwa mujibu wa Msigwa ni kuwa utaratibu huu umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama kwa serikali katika zoezi la anuani za makazi ambapo awali serikali ilipanga kutumia shilingi bilioni 740 kufanikisha zoezi hilo kabla ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuelekeza kuwa zoezi hilo litumie bilioni 28 pekee.
Hadi sasa utekelezaji wa zoezi la anuani za makazi umevuka malengo yaliyowekwa na linaendelea kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa.